Breking New

Usajili Simba Msimu huu, Hawajalala!

 


YANGA imeanza kushusha vifaa kwa ajili ya msimu ujao, lakini Simba sio kama imelala, wao wanafanya mambo yao kimyakimya na wakacheka sana kusikia wakihusishwa na straika Makusu Mundele wakisema levo hizo wameshatoka na sasa wako mbali na wanafikiria nchi za Latin Amerika.

Simba imekuwa ikielezwa inasaka winga moja matata na mshambuliaji wa kuwaongezea nguvu zaidi kina John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere ambao msimu huu wameifungua mabao 39 kati ya 73 ya timu yao katika Ligi Kuu Bara, huku ikihusishwa na nyota kadhaa kutoka nje ya nchi.


Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kwamba kikosi chao sio kwamba hakitasajili, ila hawafanyi mambo kwa presha na kwamba wanatafuta mashine sahihi kwa ubora wao ili wazidi kupaa kimataifa.


Try Again ambaye ni mmoja wa watu wazito na wakongwe katika uongozi wa Simba, alisema kwa sasa wako mbali na mawindo yao ni kutafuta mastaa wakubwa kutoka Latin Amerika inayohusisha nchi za Brazil, Ecuador, Colombia, Paraguay, Uruguay na Argentina.


Bosi huyo alisema kikosi chao cha sasa kilivyo tu kina uwezo wa kuendelea kupambana katika mashindano ya ndani, lakini bado wanataka kupata mafanikio zaidi katika mashindano ya Afrika ambayo yanahitaji watu wenye ubora zaidi.


“Tunasikia wachezaji wengi wanahusishwa na Simba, huwa tunacheka sana kuna baadhi ya majina ukiyasikia, Simba hatuko huko kwa sasa sisi tunafikiria mambo makubwa zaidi, hao wachezaji mnaowataja sio wetu tena ni wa timu nyingine,” alisema Try Again.


“Wapo, ndio wachezaji ambao tunaweza kuja kuwasajili hapa Afrika ambao hawatazidi wawili, lakini ukweli ni kwamba sasa tunatafuta watu bora zaidi kutoka huko Amerika, watu wenye kitu cha zaidi ya hawa tulionao.


“Sisi hapa ndani kwa kikosi tulicho nacho tunaweza kuendelea kushindana na timu yoyote na tukafanikiwa, hii kufungwa na Yanga juzi tunajua mambo gani yamesababisha tupoteze ambayo kama uongozi yametusikitisha sana.”


Try Again aliongeza kwa kusema: “Tunataka kupata mafanikio makubwa zaidi huko nje Afrika, lakini ili tuwe na ubora huo wa kupambana zaidi ndio maana tunakwenda huko Amerika kutafuta watu bora zaidi ambao sio rahisi pia kuwapata kwa gharama zao, ila Simba hii itapigana vita hiyo.”


Hata hivyo, haitakuwa mara ya kwanza kwa Simba kusajili wachezaji kutoka Latin Amerika, kwani msimu uliopita ilikuwa na Wabrazili watatu - straika Wilker Da Silva aliyetoka UA Barbarense ya Brazil, kiungo Gérson Fraga Vieira kutoka Atletico De Kolkata ya India na beki wa kati, Tairone Santos da Silva kutoka Atlético Cearense pia ya Brazil ambao hawakudumu ndani ya Msimbazi.


Aidha, Try Again aliongeza kwamba wapo wachezaji wa ndani watawasajili, lakini wengi wao ni wale watakaokuja kuwa kizazi cha baadaye ambao pia hawatakuwa wengi.


“Wapo wachezaji wetu hawatakuwa na muda wa kucheza kwa muda mrefu zaidi sasa, wapo wachezaji wa ndani ambao tutawasajili lakini tutachukua vijana wenye uwezo ili waje kuwa kizazi cha baadaye, ingawa nao tutachukua wale waliothibitisha ubora wao.”


ISHU YA MORRISON


Kwenye mitandao ya kijamii kuna kelele kwamba mshambuliaji wao, Bernard Morrison ameikimbia timu hiyo katika safari yake na kurudi kwao Ghana, lakini Try Again amekanusha hilo akisema Mghana huyo hana shida na ameondoka kwa ruhusa.


“Morrison hajatoroka wala hana tatizo, kocha wetu amempa nafasi ya kwenda kupumzika na atarejea. Unajua ligi imechelewa kuisha na tunaona hakutakuwa na nafasi ya kutosha sana wachezaji kupumzika na ndio maana anawapa mapumziko kwa mafungu,” alisema Try Again.

No comments